Hotuba ya Mugabe Addis imeibua mawazo kinzani: Je kafanya nini akiwa kama mwenyekiti wa AU?

February 3, 2016 § 2 Comments

Hotuba ya Rais Robert Mugabe kule Addis wakati wa kumaliza kikao cha viongozi wa Afrika imevuta hisia mchanganyiko kwa watu mbali mbali. wengine tumefurahia kuona Mugabe bado ana ujasiri wa kuwakandia wazungu. Wengine tuna “reservations”. Nikaona ni vizuri nitoe maoni yangu. Mengi nimeshayasema kwenye kurasa za marafiki zangu lakini nimeonelea niyakusanye na kuyaweka hapa pamoja pia.

Mwanzoni niliposikia hotuba ile nilipatwa na mawazo mchanganyiko mawili. Kwanza niliona yes Mugabe ni shujaa anaweza kusema ukweli kama ulivyo. Ikiambatana na hilo nikaona pia kudai kiti katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ni haki yetu na kuomba Umoja wa mataifa ufanyiwe matengenezo (reforms) ni sahihi. Upande mwingine ukanishawishi kuangalia record ya mzee Mugabe na kulinganisha na ukali wa maneno yake juu ya nchi za magharibi zilizokuwa zikimtaka atoke madarakani. Nikaona picha pia ya jinsi uongozi ng’ang’anizi ulivyoiletea madhara nchi yake. Nikasikia pia alivyomsifia Mwalimu na mchango wake katika ukombozi wa Afrika akitahadhari kuzungumza upana wa falsafa za Mwalimu. Nikagundua kuna tatizo kubwa kwa Mugabe na Afrika yetu.

Kuna watu tunafurahia sana lugha za kutukana wengine tukisikia mtu anatukanwa na hasa mzungu tunafurahi sana. Kwa kanuni aliyotufundisha Mwalimu hotuba ya Mugabe kule Addis haikuwa nzuri. Kutumia kauli za kibaguzi kama “white faces na pink noses” kwa maoni yangu si mujarabu hata kidogo. Na hatupaswi kushangilia. Sisi tuliwachukia wakoloni si kwa sababu ya rangi yao bali kwa vitendo vyao. hatupaswi kabisa kulipiza kwa kauli za kibaguzi namna ile. Baraza la usalama halina wazungu peke yake wako wachina pia. Alipogundua kwamba yuko Ban Ki Moon pale akaanza kubadili kauli jambo ambalo ni unafiki. Lakini kwa sababu aliyetukanwa ni mzungu tunafurahia. vitendo anavyowafanyia wazimbabwe si vizuri na kiburi anachowajengea viongozi wa Afrika cha kung’ang’ania madarakani si jambo jema kwa bara letu.

Anamsifia Nyerere lakini hataki kuishi kanuni zake. Mugabe ni hatari kwa Afrika. Alikuwa amejiwekea rekodi nzuri lakini yote kaiharibu hafai kuigwa. Kupigania kiti kwenye Baraza la Umoja wa mataifa hakusaidii chochote Afrika isiyokuwa na umoja, isiyoweza kutatua matatizo yake yenyewe. Afrika inatakiwa kwanza itengeneze sauti yake, ikisema kitu dunia ielewe Afrika imesema. Afrika imeshindwa hata kutengenza umoja imara wa kikanda. Afrika bado inaamini katika vinchi vidogo vidogo ambavyo ni vichaka vya madikteta wanaokutana Addis na kufanya matamko yaliyojaa hewa tupu hayana madhara. Badala ya kuendelea kuwaaminisha watu kwamba matatizo yetu si kwa sababu yetu wenyewe na viongozi wetu Mugabe anataka tuamini kuwa matatizo yetu ni kwa sababu hatuna kiti katika baraza la usalama la umoja wa mataifa ni upuuzi uliopitiliza.

Kuna damu za waafrika zinamwagika Burundi, DRC, CAR, Libya, Somalia na shida ya Boko Haram Nigeria ilyosambaa kwa majirani wote. AU imeyafanyia nini? Kama mwenyekiti wa AU Mugabe kasaidia kitu gani Burundi? Hivi kati ya suala la Burundi na kesi ya kina Ruto kule ICC kipi ni muhimu zaidi kwa Afrika? Kinachoendelea Burundi ni dhahiri kuwa Warundi wenyewe hawataweza kuutatua ule mgogoro. Nkurunzinza na wenzake walioko madarakani wataendelea kuua wapinzani. Leo Tanzania tuna wakimbizi zaidi ya laki moja kutoka Burundi kwa sababu ambazo Afrika ingeweza kuzuia. Mugabe ame-deliver nini katika term yake kama mwenyekiti wa Afrika? Viongozi wanatumia kodi zetu kusafiri na kukutana Addis kufanya nini cha mno ambacho kina mguso kwetu?

Katika mojawapo ya hotuba za Mwalimu akiwa kiongozi wa Tume ya kusini (South – south Commission) alisema wazi kuwa kizazi cha pili cha viongozi wa Afrika kilikuwa na jukumu la kuleta umoja wa Afrika ili bara la Afrika liwe na sauti moja duniani. Alisema tukiwa na sauti moja tuna nafasi nzuri ya kusikilizwa. Sasa tangu Mwalimu aliposema tumekuwa na vizazi (vya uongozi) vitatu na hiki sasa cha nne njozi ya umoja iko mbali hata kuliko wakati wa waasisi wa wa Afrika (kina Kwameh Nkurumah, Julius Nyerere, Jomo Kenyatta, Haile Selasie, Gamal Abdel Nasser, nk) mwaka 1963. Nikiwa Darasa la tano Mwaka 1981 ndipo African Economic Community (Jumuia ya uchumi ya Afrika). Leo ukiwazungumzia kizazi cha sasa wanakushangaa! Bado waafrika tunatumia passport kwenda nchi nyingine, ukikutwa nchi nyingine bila “makaratasi” unafukuzwa, huu uchumi wa pamoja itakuwaje? Ni nini kinatuzuia Africa kuwa shirikisho lenye nguvu la kiuchumi? Halafu leo nimsifie Mugabe kwa maneno rahisi ya kutafuta umaarufu kwa wasikilizaji? Hapana?

Advertisements

§ 2 Responses to Hotuba ya Mugabe Addis imeibua mawazo kinzani: Je kafanya nini akiwa kama mwenyekiti wa AU?

    • kadulyu says:

      Asante Tumaini; unajua Kama waafrika hatutakuwa tukiambizana ukweli na hasa juu ya viongozi wetu wataendelea kuona AU ni mali yao. Wananchi wa Afrika tumejiweka mbali sana na chombo hiki muhimu cha kutuunganisha. Kodi zetu ndio zinazowasafirisha na kugharimia mikutano yao, badala ya kushughulikia mambo yanayogusa Wananchi wao wanashughulika Na mambo Yao binafsi kama kulindana.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

What’s this?

You are currently reading Hotuba ya Mugabe Addis imeibua mawazo kinzani: Je kafanya nini akiwa kama mwenyekiti wa AU? at kadulyu.

meta

%d bloggers like this: