Zitto and Chadema leadership failed to capitalize on the dividends of the law of concentration in politics
March 10, 2015 § Leave a comment
Aliyewahi kuwa mpiganaji wa mstituni, Rais maskini kuliko marais wote duniani: Rais wa Uruguay ndugu Mujica aachia madaraka
March 3, 2015 § 1 Comment
Imechapishwa: March 01, 2015 12:36
Imeandikwa mwanzo na Reuters/Andres Stapff
kutafsiriwa na kadulyu.wordpress.com March 2, 2015
Rais wa Uruguay, Jose Mujica, almaarufu ‘Pepe’, ambaye aliwahi kuwa mpiganaji wa msituni, ambaye muda wote amekuwa akiishi katika shamba lake amekuwa akitoa sehemu ya mshahara wake kwenye shirika la misaada, sasa ameachia madaraka baada ya kutawala miaka mitano, amekamilisha muhula wake akiwa mmoja wa viongozi maarufu sana duniani.
Mujica, (79), anaondoka madarakani akiwa na ukubali wa asilimia 65 ya watu wa Uruguay. Ameheshimu katiba inayomzuia kugombea vipindi vinavyofuatana.
Yeye anasema, ‘Nilipoanza kuwa rais nilijaa nadharia, lakini baadaye ukweli uligonga’, alisika akisema alipohojiwa gazeti la wiki hii la AFP.
Baadhi humwita “Rais maskini kuliko wote duniani”. Wengine, “Rais ambaye kila nchi wengependa wawe naye”. Lakini Mujica husema, “Bado kuna mengi ya kufanya” na ana matumaini kwamba serikali ijayo, itayoongozwa na Ndugu Tabare Vasquez (Ambaye kachaguliwa kwa mara ya pili Novemba mwaka jana) atakuwa, “bora kuliko mimi na atakuwa na mafanikio makubwa”
Mujica amefanikiwa kuiweka Uruguay katika ramani ya dunia. Amefanikiwa kuibadili nchi ya wafugaji ya watu milioni 3.4 kuwa nchi inayouza nishati nje, Brazili ikiwa nchi inayoongoza kama soko lao (ikifuatiwa na China, Argentina, Venezuela na Marekani).
Uchumi wa Uruguay wa Dola za kimarekani billion 55 umekuwa ukikua kwa asilimia 5.7 kila mwaka kuanzia mwaka 2005, kwa mujibu wa benki ya dunia. Deni la Uruguay likilinganishwa na pato la taifa (yaani uwiano kati ya deni na patoa la taifa – debt-to-GDP ratio) limekuwa likipungua kutoka asilimia 100 mwaka 2003 hadi asilimia 60 mwaka 2014. Kwa muda huo pia gharama za deni hilo zimepungua pia ikiwemo matumizi ya dola kutoka asilimia 80 mwaka 2002 hadi asilimia 50 mwaka 2014. Takwimu hizi bila shaka zinadhirisha taifa linaloongozwa na mtu makini.
Mwenyewe anasema, “Tumekuwa na miaka chanya ya usawa. Miaka kumi iliyopita Waurguay asilimia 39 waliishi chini ya kiwango cha umaskini; tumeshusha kiwango hicho hadi asilimia 11 tu na tumepunguza watu wanaoishi katika umaskini uliokithiri kutoka aslimia 5 hadi 0.5”.
Baada ya kushindwa kwa jitihada za nchi za Amerika ya kusini kwenye vita dhidi ya madawa ya kulevya, nchi hii ya Amerika ya kusini ikawa nchi ya kwanza duniani kuhalalisha matumizi ya bangi, Mujica alisimamia hoja kwamba biashara ya madawa ya kulevya ni hatari zaidi ya bangi yenyewe. Huo ndio ulikuwa msimamo wake sie kwetu hapa bangi ng’o. Japo nasikia kuna watu wametajirika sana na bangi hapa kwetu Tanzania.
Kwa kweli ni miongoni mwa marais wenye upeo mkubwa katika eneo la Amerika ya Kusini. Ingawa Mujica amefanya mambo mengine ambayo hayakubaliki katika jamii na imani zetu kama kuhalalisha ndoa za jinsia moja, amekuwa rais wa kwanza kuwakubali wazuiwa wa Guantanamo Bay kule Cuba. Wazuiwa wa Marekani 6 ambao walikuwa hawajashitakiwa kwa kosa lolote walikaribishwa Uruguay kama wakimbizi. Hawa walikuwa Wasyria wanne, Mpalestina na Mtunisia. Ingawaweje waliruhusiwa kuachiwa tanu mwaka 2009, Marekani haikuwaachia hadi pale rais wa Uruguay alipokubali kuwapokea.
(Reuters/Andres Stapff)
Ndani ya mafanikio hayo na utata katika maamuzi hasa ya mambo ya kijamii, tukumbuke kwamba rais Mujica alikuwa kiongozi wa wapiganaji waasi wa msituni wa mrengo wa kushoto, alifungwa miaka 13 jela wakati wa utawala wa kidikteta na kijeshi. Alihimili mateso na miezi mingi ya kuwekwa upweke. Lakini pamoja na yote Mujica anasema hajutii muda wake gerezani bali anaamini ulimsaidia kujenga tabia yake. Wengi leo ugumu tunaulaani japo wakati mwingi hutusaidia kutujenga. Raha maisha yote ya ujana, kula kulala havijengi vinaharibu.
Ukarimu wa Rais Mujica unaongea mengi na makubwa: Alikataa kuhamia Ikulu ya kifahari ya Uruguay ambapo ndio makao rasmi ya Rais, badala yake akachagua kuishi shambani mwake nje ya mji wa Montevideo akiwa na mkewe na mbwa kilema wa miguu mitatu. Pepe kama anavyojulikana alitoa asilimia 90 ya mshahara wake mfuko wa misaada kwa maskini akisema hakuhitaji mshahara huo. Anaendesha gari aina ya Volkswagen Beetle ya mwaka 1987!
Mwaka jana, Mujica alikataa ofa ya dola millioni moja kutoka kwa shehe wa kiarabu alotaka kununua gari lake. Pepe alikataa kuuza gari yake hiyo akisema, atawaudhi, ‘Marafiki zake ambao walichangia kuwanunulia hilo gari”
Alivyo mtu wa pekee kuna siku moja aliwahi kusimama na kumpa lifti kijana aitwaye Gerald aliyekuwa amesimama pembeni akiomba lifti. Aliposhushwa alishukura sana na kushangaa kupewa lift na rais wa nchi maana wote walimpita lakini yeye alisimama na kumsaidia.
Mwisho
Kiongozi bora ni yule anayemaindi mabadiliko chanya ya watu na nchi yake na si yule anayeangalia mabadiliko yake tu. Viongozi wengi wameshindwa kuleta mabadiliko katika nchi zetu kwa tamaa tu ya kutajirika utajiri ambao kiuhalisia hatuendi nao popote. Wakati huu watu wanapofikiria kuwa viongozi katika ngazi mbalimbali wajihoji nia hasa yao nini? Ni kusavaivu tu kwa sababu hawana namna nyingine ya kuishi ama wanajitoa kwa ajili ya nchi yao hata kama wao watakufa maskini lakini potelea mbali nchi isonge? Ufisadi ambao tumekuwa tukiushuhudia kwa viongozi wetu kila kukicha unatisha na hauleti matumaini ya ama muda mfupi au mrefu. Ni bahati mbaya sana hakuna mgombea wa urais katika wale waloonyesha nia anayeyaona haya zaidi ya kujenga mfumo wa kulindana. Nani atatoka kama Mujica wa Uruguay?
Fanya mabadiliko katika eneo lako unalolimudu (Make change within your sphere of influence)
March 3, 2015 § Leave a comment
Leo nimeenda asubuhi kwenye duka moja kubwa wenyewe mwaita supa maketi, mie mpenzi wa karanga na korosho. Kwa muda mrefu sasa nimekuwa nikienda pale kununua hizo njugu (nuts). Muda fulani uliopita niliacha baada ya kugundua ubora wa zile karanga umebadilika yaani umeshuka. Lakini basi kila wakati hupita kuona kama kuna mabadiliko chanya ya ubora wa hizo karanga. Ajabu kila ninazozikuta ni mbaya zaidi kwa maana zimeungua zaidi, uchafu mwingi na zilizooza zinaonekana wazi zaidi.
Nilipokuwa hapo leo kwa hiyo shelf nikatafakari nikaona kuwa hili jambo la kuwa naumia tu na kuondoka haifai ngoja nijaribu kuvuka kidogo msitari wa upole wangu. Mwezenu nilikuwa nimetokelezea kipamba pia na kamkia ka shingoni, si mwajua tena sie watu wa mara moja kwa mwezi! Ukiniona waweza fikiria ni miongoni mwa wale wala mboga za milioni kumi nini! hahahah!
Basi nikachukua pakiti ya karanga, nikajivalisha sura ya mamlaka kidogo (baada ya kukumbuka ule usemi mfalme sijui ni mteja ooh hapana, ‘Mteja ni mfalme) nikauliza mfanyakazi mmoja wa hapo dukani, nani mkuu wa hapa? Kanionyesha jamaa mmoja ambaye naye alikuwa kaweka kipamba chake kuonyesha kweli ni mkuu pale. Nikamfuata yapata kama mita kumi hivi kutoka kwa ile shelf, mita kumi zilinipa muda wa kupanga hoja na kuzoea mwonekano wa kimamlaka niliouvaa muda mfupi. Nilimuuliza swali moja tu, ‘Ubora wa hizi karanga unalingana na hadhi na heshima ya hili duka?’, swali lililofuata, ‘Hili duka kubwa mna mpango gani wa kusaidia wajasiriamali kuinua ubora wa bidhaa zao?’
Yule mkuu nikaona kashtuka na kupata woga hivi. Nikarekebisha kidogo uimla niliomwingia nao. Akachukua ile bidhaa tukafuatana naye kwenye ile shelf, kila akiokota pakiti tatizo ni lilelile. Ndipo aliponigeukia na kuniomba radhi sana. Na kushangaa eti kupata mteja mkweli na jasiri wa kusema kisichomfurahisha. Na akakiri kwamba ni kweli hiyo bidhaa haiendi siku hizi. Mwisho niliona wanaiondoa bidhaa yote kwa shelf, wakampigia muuzaji wa hiyo bidhaa aje kuichukua mara moja.
Nikawaambia ili kuleta nidhamu katika ubora wa bidhaa zetu hapa nchini ni vizuri wafanyabiashara wa kati wawe wanaelekeza wajasiriamali wetu kuweka na kuheshimu viwango fulani vya ubora. Hii itatusaidia kuinua ubora wa bidhaa zetu hata zionekane zinafaa kuuzwa nje pia. Kwa nini isiwezekane? Kitu kingine nikajifunza kumbe wote tungechukua hatua katika mdura wetu wa mvuto (our sphere of influence) tunaweza kuleta mabadiliko. Na ujumla wa mabadiliko madogo madogo ya sisi wanyonge yatajijenga na kuwa mabadiliko makubwa tena ya kudumu (sustainable changes). Naitoa hii stori ya kweli kwa wote wapenda mabadiliko.