Sheria isimamiwe kutenda haki kwa usawa kati ya watawala na watawaliwa, wenye nacho na wasio nacho

February 11, 2015 § Leave a comment

Kama wananchi hawatasimamia kupata katiba bora na kuwaachia tu wanasiasa ambao hasa nia yao ni kuimarisha madaraka kandamizi kwetu, tutaendelea kunyanyaswa ndani ya nchi yetu. Nchi inaendeshwa kiajabu sana. Watawala wao tu ndio wanajifikiria ndiyo nchi, wanatukumbuka kuwa na sie tupo mara moja kila baada ya miaka mitano. Mwaka huu watatukumbuka na watapita hata majumbani mwetu kutushawishi tujiandikishe, tupige kura na kadhalika. Lakini kiuhalisia si eti tujiandikishe bali tujiandikishe ili tuje tuwapigie kura wao. Wakishika patamu wanatuaona sie nongwa na kutoa matamko ya kutunyanyasa. Sisi ndio wahalifu wao ni malaika. Sisi tukikosa tuadhibiwe tena papo kwa papo, wao uhalifu dhidi ya uchumi wetu ndiyo madaraja ya kupatia ubunge na hatimaye uwaziri ili waendelee kujipendelea. Tumependekeza Wabunge wasiwe mawaziri, tumeona walivyoshtuka!
Ndugu yangu Francis Cheka – Bondia aliyeiletea heshima nchi yetu juzi kafungwa miaka 3 kwa kumpiga makonde ndugu mmoja pale Morogoro. Alijisahau akadhani yuko ulingoni. Alifanya kosa na anastahili adhabu. Mzee wangu Andrew Chenge kagonga na kuua wadada wawili usiku akiendesha gari kizembe na isiyokuwa na bima, alifanywa nini? Sipendi kuingilia uhuru wa mahakama lakini jambo la wazi kabisa hapa kwamba sheria zetu zinaundwa, kutekelezwa na kusimamiwa kwa namna ambayo ama kwa makusudi au kwa namna zilivyoundwa na mfumo wake, zinawatendea tofauti wenye nacho na wasio nacho.
Hata kwa hizi tuhuma za ulaji wa Pesa za umma zilichotwa kutoka akaunti ya Tegeta Escrow watuhumiwa hawatendewi kwa usawa. Baadhi ya waliopokea hizo pesa wamefikishwa mahakamani tayari. Baadhi yao hasa wakubwa (mfano Mh. Prof Tibaijuka, Chenge tena, majaji wale wawili, n.k) wanakula bata mtaani. Mapema Mkuu wa PCCB alipoulizwa kwa nini hawa wengine hawafikishwi mahakamani alisema hao hadi DPP ambaye naye lazima aruhusiwe na Rais ndio wanaweza kukamatwa. Nilishangaa sana maana tayari Mwanasheria mkuu ndugu Werema, Prof Tibaijuka na sasa Prof Muhongo si wateule wa Rais tena, kwa nini sheria isifuate mkondo wake? Mbona wazee wangu kina Basil Mramba na Yona wanajibu kesi mahakamani kwa uzembe wa kuisababishia serikali hasara? Mahakama, Magereza na polisi si kwa ajili ya watu wa chini tu ni kwa ajili ya wote.
Katika nchi inayoheshimu utawala wa sheria hakuna mtu ambaye yuko juu ya sheria. Kiongozi akivunja sheria awe wa kisiasa au kiserikali avuliwe madaraka mara moja ili sheria imtendee haki pia. Kuadhibiwa kwa mkosaji ni sehemu ya haki. Kuwaachia wahalifu wakiranda mitaani eti kwa jeuri ya vyeo, umaarufu wao au pesa zao ni ubakaji mkubwa wa haki. Utofauti wetu wa kipato usiende hata kwenye sheria, kwamba sheria zinatungwa kwa ajili ya watawaliwa na si watawala. Labda nikurejeshe kidogo kwenye CCM ya zama zile:
CCM kilikuwa ni chama cha wakulima na wafanyakazi kilichojengwa kwa misingi ya usawa, haki na maadili si chama cha kuvumilia na kuchukuliana na watu wasio waadilifu. CCM ilikuwa na imani na imani yake ilikuwa katika siasa ya ujamaa na kujitegemea. Nilihudhuria madarasa kujifunza itikadi na mfumo wa chama kabla sijakabidhiwa kadi ya uanachama na kuapa kwa ahadi hizi:
  1. Binadamu wote ni ndugu zangu na Afrika ni moja.
  2. Nitaitumikia nchi yangu na watu wake wote
  3. Nitajitolea nafsi yangu kuondoa umaskini, ujinga, magonjwa na dhuluma.
  4. Rushwa ni adui wa haki. Sitapokea wala kutoa rushwa.
  5. Cheo ni dhamana. Sitakitumia cheo changu wala cha mtu mwingine kwa faida yangu.
  6. Nitajielimisha kwa kadiri ya uwezo wangu na kutumia elimu yangu kwa faida ya wote.
  7. Nitashirikiana na wenzangu wote kuijenga nchi yetu.
  8. Nitasema kweli daima, fitina kwangu mwiko.
  9. Nitakuwa mwanachama mwaminifu wa CCM na raia mwema wa Tanzania na Afrika.
  10. Nitakuwa mtiifu na mwaminifu kwa Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ambazo leo zimegaragazwa mavumbini. Angalia ahadi ya 3, 4, 5 na ya 8 na 9 halafu uniambie kama Wabunge wenye tuhuma za wazi za ufisadi kama wa akaunti ya escrow, chenji za rada, wachukua rushwa kutoka serikali za mitaa tena wakiwa wameshikwa na hela za moto, bado hadi leo ni wanachama wa CCM na wabunge. Halafu tunataka kuaminishana kweli chama chetu kiko na nia ya dhati ya kupambana na rushwa?? HAPANA! HAPANA! HAPANA!
Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

What’s this?

You are currently reading Sheria isimamiwe kutenda haki kwa usawa kati ya watawala na watawaliwa, wenye nacho na wasio nacho at kadulyu.

meta

%d bloggers like this: