Waraka wa VIPEM kwenye vyombo vya habari unazua maswali zaidi

November 26, 2014 § Leave a comment

Ndugu Watanzania,

Nimesoma (nadhani taarifa kwa umma) ya VIP Engineering and Marketing Ltd kwenye gazeti la Mwananchi toleo namba 5238 la 25/11/2013, Uk 7. Ikiwa na kichwa, ‘ NANI ANACHEZESHA NGOMA YA ESCROW’. Najua ni taarifa ndefu lakini isomeni ili pia kupata habari upande wa pili kutimiza ile tunaita natural justice tunavyomhukumu mtu kimaoni.

VIP wamejitetea sana katika taarifa hii. Kwa walio wengi umiliki wa IPTL na uhusiano wake na VIP Engineering and Marketing vinaweza kutuchanganya kidogo. Nitajaribu kuelezea vile ninavyofahamu ili hasa kujua kwa nini VIP Engineering wanajitosa kujibu hoja za wananchi kuhusu sakata la account ya udhamini (escrow account) ya Tageta. VIPEM walifanya ubia na shirika la Mechmar la Malaysia, VIPEM asilimia 30 na Mechmar asilimia 70 na kuunda Kampuni iitwayo Independent Power Tanzania Limited (IPTL). Kuna maswali kama, Je, wabia hawa walilipia share zao kiasi gani? Je, zilikuwa ngapi na zenye thamani gani kila moja? Faida iliyopatikana kwa mwaka waligawanaje? Gawio hutozwa kodi, walilipa kodi kiasi gani hawa wabia tangu walipoanza kufanya biashara miaka ya 90 hadi leo? Iweje hadi mwaka 2013 VIPEM walikuwa hawajapewa gawio lao hadi wasubiri pesa za akaunti ya udhamini ya Tegeta?

Turudi kwenye taarifa ya VIPEM ya tarehe 25/11/2015 kutoka kwenye gazeti la Mwananchi  kwa umma. Ninayoyaona kwenye taarifa ni haya yafuatayo :

  1. VIPEM wanamtetea Prof Anna Tibaijuka ambaye vyombo vya habari vimeripoti kupewa Shs 1.6bil na mkurugenzi wa VIPEM. Kinachosemwa kuhalalisha mgao huu eti VIPEM walikuwa wanatoa mchango wao kwa shule anayoindesha Prof Tibaijuka na eti kwa sababu ana-promote elimu kwa watoto wa kike. Na taarifa inadai Prof alikuwa ameomba kwa maandishi mchango huu kwa muda mrefu na hivyo VIPEM walipopata gawio lao kupitia akaunti ya udhamini ya Tegeta (escrow account), wakaona ndio wakati mwafaka kuchangia elimu.
  1. Anasema saga Hii ni kwa sababu ya benki ya Standard Chartered kutaka zile hela za escrow ingelipwa yenyewe Kwa madai iliyo nayo kwa kwa kuwahi kuwakopesha IPTL. (hazungumzii kwa nini IPTL ilikuwa hailipi deni lake kwa benki hiyo)
  1. Jambo la escrow account linachochewa na Stanchart bank na eti ndiyo inayotoa information kwa vyombo vya habari.
  1. Anazitetea Mahakama za hapa
  1. Anadai pesa zilizokuwa kwa escrow account si mali ya umma

Hayo ni machache niliyoyaona. VIP wanashindwa kutuambia yafuatayo:

  1. Ukirejea hoja namba moja hapo juu, kutokana na gazeti la Mawio ambalo hakuna aliyekanusha pesa hizi zililipwa kwa account binafsi ya Prof Anna Tibaijuka. Je, hii Shule ya Babro Johanssson haina akaunti yake benki? Je watoto wakisoma ada hulipa kwa Prof au kwa shule? Prof Tibaijuka ni mtu mwenye elimu ya juu sana wenyewe wanaita Uzamivu yaani PhD ya mambo ya uchumi na pia ni mtumishi mwandamizi wa umma, hivi hajui kutofautisha kati ya shughuli binafsi na kampuni au shirika?
  1. Kama hiyo haitoshi inasemekana pesa hizi za escrow zimegawiwa kwa mtu wa RITA (ambaye alikuwa akisimamia ufilisi wa IPTL), Zimelipwa kwa mfanyakazi mwandamizi wa TRA (ambaye juzi Naibu Waziri wa Fedha aliagiza afukuzwe kazi na akaunti zake zishikiliwe), zimelipwa kwa majaji wawili na mmoja wao ni Professor (nadhani yuko EAC siku hizi) na amekiri kupokea zaidi ya million 400, Mawaziri wa zamani wa Nishati na Madini, na wengine wengi . Amewapa hayo mamilioni aliwapa kwa sababu gani? VIPEM wamekwepa kuzungumzia hayo badala yake wamejikita kumtetea Professor Tibaijuka pekee. Kuna nini hapo?
  1. Kwa nini hizi pesa zitolewe kabla ya kesi ya pingamizi kuamriwa na mahakama? Kesi ya msingi imemriwa February 2014. VIPEM katika habari yake kwa umma haizungumzii kwa nini walisukuma kupewa hizi pesa zilizokuwa chini ya mdhamana badala ya kusubiri maamuzi ya kesi. Hazungumzii ni nini walifanya hadi watendaji wa serikali wakatoa vibali vya kuchota hizo pesa.
  1. Malalamiko ya msingi ya Tanesco ni IPTL kutoza kiwango uwezo cha kuzalisha umeme ‘capacity charges’ cha juu kuliko fomula ya makubaliano. Gharama hizo zinakokotolewa kutokana na gharama za mwanzo za uwekezaji. VIPEM hazungumzii kwamba gharama iliyopita kiwango ilitokana na IPTL kuumua/kuongeza (inflate) gharama za mwanzo za uwekezaji (ujenzi wa kituo, gharama za mitambo/aina ya tekinolojia n.k) na pia Kwa nini IPTL ikajenga mitambo ya mwendo kati (medium speed) badala ya mwendo pole (slow speed) kinyume na mkataba na Tanesco? Haya yote waraka huu umekwepa kuyazungumzia.
  1. Kudaiwa na benki kama umekopa ni kitu cha kawaida. Kwa nini waraka haulezi hali ya mahusiano kati ya wawekezaji VIPEM, Mechmar na benki ya Standard Chartered? Waraka unasema, ‘Baada ya VIPEM kuuza hisa zake kwa PAP (Yule Singa Singa Sethi) na kulipwa stahili yake…’ Je, VIPEM alilipwaje stahili yake? Inavyosemekana yule singa singa amenunua IPTL kwa shs milioni 6 na hakulipa kodi. Alipataje Mabilioni ya kumlipa VIPEM kama si zile pesa za escrow zilichotwa kwanza na kugawanwa bila kujali kesi ya Tanesco vs IPTL? Material facts ziko wazi kwamba ile kesi lazima Tanesco wangeshinda kwa hivyo VIPEM na PAP wakatumia ujanja walioujua kulipwa kabla ya maamuzi ya kesi.
  1. VIPEM waelewe kuwa maslahi ya nchi hayaangaliwi na viongozi aliowaita wawili wenye nia mbaya. Tunayaangalia sisi sote wananchi wapenda maendeleo, na hatukubali, iwe Standard Chartered Bank, PAP, VIPEM au yeyote kukwepua mali ya umma. Ninasema hivyo kwa sababu katika waraka huu VIPEM wanajenga hoja indirectly kwamba hizi pesa kuchukua wao ni sawa lakini kuchukuliwa na Standard Chartered Bank si sawa kwa kuwa wao si wazalendo.
  1. VIPEM anadharau kwamba pesa za escrow si mali ya umma ila ziliwekwa pale kutokana invoice (madai) ya IPTL kwa Tanesco. Kutokana habari tunazozipata ambazo hazijakanushwa ripoti ya CAG inaonyesha tayari Tanesco kabla ya kesi walikuwa wamewalipa IPTL zaidi ya billion 320 na pale akaunti ya udhamini (escrow account) kulikuwa na bilioni 306 ambazo tayari zimechotwa, hizi pesa ilikuwa zirudi Tanesco na IPTL wadaiwe bilioni 15 halafu baadaye ndiyo Tanesco waanze kulipa ‘capacity charges stahili. Kila mwenye akili timamu hahitaji kwenda shule hata ya kindergarten kujua kwamba pesa za escrow zilikuwa ni mali ya umma.
  1. Madai kwamba IPTL ilikuwa inatoza capacity charge ndogo kuliko makampuni mengine yanayoiuzia umeme Tanesco. Hiyo ni kweli na sisi wananchi haturidhiki na ndiyo maana ishu ya Richmond ilimwondoa Mheshimiwa Lowassa Uwaziri Mkuu. Lakini si hoja halalishi (pretext) ya IPTL kutoza capacity charges zaidi ya kiwango kulichokubaliwa kimkataba. Nasisitiza kama hapo juu mkataba wa Tanesco na IPTL uko wazi kwamba capacity charges zitakokotolewa kufuata gharama za mwanzo za uwekezaji na si kwa kulinganisha na makampuni mengine. Kwanza enzi zile wala hayo makampuni hayakuwepo.
  1. VIPEM analaumu magazeti, anasema yanahukumu. Magazeti ni sauti ya watu na mahala pengi yamesaidia kuongeza uwajibikaji wa viongozi. Kuyabeza magazeti ni kutowatendea haki wananchi wa Tanzania. Cha msingi VIPEM waelewe kuwa vyombo vya habari vinaweza kupata chanzo cha habari kutoka popote na vinafuata misingi ya taaluma kutenda kazi zake. Ikiwemo na ‘triangulation of sources of information’ yaani kuthibitisha habari kwa kutumia vyanzo kadhaa. Magazeti yetu ya Mwananchi, The Citizen, Nipashe, Mawio, Mitandao ya Jamii kama Jamii Forum, Wanabidii, Mwahalisi Forum, n.k, vyombo hivi vinanaendeshwa kwa ueledi mkubwa na tunavipongeza kwa juhudi za kufichua vichaka vya ubadhirifu vinavyotesa nchi yetu. Vyombo vya habari viko wazi kwa wote hata kwao VIPEM na PAP, badala ya kujificha kwa mgongo wa mahakama walitakiwa wawe huru kujibu hoja za wananchi juu ya uchotaji wa hizo pesa.
  1. Uanzishwaji na hatimaye uzalishaji wa umeme na uendeshwaji wa IPTL umekuwa na utata tangu mwanzo. VIPEM ilitegemewa kama kampuni ya M/Watanzania kuwa mbele kuonyesha kuwa na sisi tunaweza badala ya kufikiria maslahi binafsi mbele zaidi. Kugawa mabilioni hayo kwa wanasiasa na watendaji wa serikali kwa sababu ambazo hata zingekuwa halali inaleta maswali kwenye falsafa ya uendelevu wa biashara (business sustainability) na haitufundishi sisi wajasiriamali kuzingatia maadili tangu mwanzo wa biashara zetu.

Hivyo basi kama haya maelezo katika toleo la 25/11/2014 la mwananchi ndiyo ukweli wa VIPEM na PAP wanaousimamia kutetea uchotaji wa fedha za umma bado unazua maswali mengi kuliko majibu na wananchi bado tunataka hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi ya kila aliyehusika na pia fedha zote zirudishwe.

Saini tamko kukataa vitendo vya ufisadi na wahusika kuchukuliwa hatua za kisheria:

https://secure.avaaz.org/en/petition/Wito_kwa_Wabunge_na_Rais_wa_Jamhuri_ya_Muungano_wa_Tanzania_WITO_WA_KUHAKIKISHA_UWAJIBIKAJI_KAMILI_UNATENDEKA_NA_PESA_ZA/?nvEMffb

Where Am I?

You are currently viewing the archives for November, 2014 at kadulyu.