Tutafakari namna ya kushughulikia matukio ya uhalifu wa kutumia pikipiki

October 24, 2014 § Leave a comment

Uhalifu unaofanywa kwa kutumia pikipiki unazidi kushamiri Dar. Pikipiki inarahisisha wahalifu kutoroka. Je, tufanyeje kumaliza hili tatizo?

Pikipiki ni nzuri kwa kufanyia uhalifu kwa sababu zinasaidia kutoroka haraka, zinaweza ku-meander kwenye foleni na kumudu changamoto za msongamano wa magari hapa Dar, zinaweza kupita uchochoroni na zina speed ya kutosha kuiacha hata gari. Naamini hii ndio sababu pekee kwa nini wahalifu wanatumia aina hii ya usafiri kwa sasa.

Tukio la Mlimani City la kuuawa kwa ndugu Cheyo, la juzi pale bakery ya Kawe/Mlalakuwa na la kuuawa kwa yule mtawa akiwa njiani kupeleka fedha benki na hili la jana pale Stanbic Mayfair na mengine mengi yanafanana. Kwa mujibu wa mashuhuda inasemekana kwamba wale majambazi walioiba Stanbic walikuja wengine ndani ya gari aina ya Noah na wengine wawili wakiwa juu ya pikipiki na silaha walipaki nje mkabala na hiyo benki na wawili waliingia ndani na silaha kwenda kufanya uhalifu huo.

Hapo zamani Benki walikuwa wakizuia magari ya aina fulani kuegesha maeneo ya benki. Siku hizi huo utaratibu haupo. Hata hivyo walinzi makini wa benki na taasisi nyeti huzuia kuegesha kwenye maeneo yao kwa mkao wa kuondoka. Watataka uegeshe kwa namna ambayo ili uondoke lazima u-reverse kwanza. Hii ina maana yake kiusalama.

Nikirejea suala la pikipiki, njia mojawapo ya kukabili uhalifu huu ni kuweka kanuni ya umbali wa kuegesha pikipiki kutoka maeneo nyeti yakiwemo na maduka kadhaa yatakayopitishwa kutumia kanuni hiyo. Au tuwe na kanuni za kuzuia watu waliobebana kwenye pikipiki kuingia maeneo ya taasisi za fedha au maduka yaliyopendekezwa. Hii ni pamoja na kuzuia mwingine kubakia juu ya pikipiki bila kuizima.

Pendekezo lingine litahusu zaidi teknolojia. Kuweka masharti juu ya specifications za pikipiki zinazouzwa Tanzania. Mojawapo uwashaji wake uwe tu wa kutumia mguu badala ya kubofya. Yote haya yana maana kiusalama.

Maisha ya watu yanapotea kirahisi, wahalifu wanaona ni jambo dogo sana kutoa uhai wa mtu. Tumeruhusu bodaboda kupatia vijana wetu ajira na kurahisisha usafiri. Lakini kuna baadhi wamejaribiwa kufikiri kukusanya elfu moja moja kutoka kwa wateja wao haitoshi wanafikiria kuwaua wateja badala yake. Serikali na vyombo vyake vya usalama walifanyie kazi hili haraka ili walau maisha ya Mtanzania mwingine yasipotee kwa njia hii.

 

Je, Hukumu aliyopata Pistorius ni ya haki?

October 22, 2014 § Leave a comment

Oscar Leonard Carl Pistorius, Mwafrika Kusini ambaye alikatwa miguu yote miwili chini ya magoti akiwa na umri wa miaka 11. Kwa jitihada za madaktari alitengenezewa miguu ya bandia na baadaye kuwahi kuwa mkimbiaji mzuri wa mbio fupi, hatimaye jana kahukumiwa kwenda jela miaka mitano kwa kosa la kumuua mpenzi wake Reeva Steenkamp mwaka jana.

Kijana Oscar amepitia kipindi kigumu cha kesi yake. Hata hivyo hukumu yake imezua maswali mengi. Hapo jana familia ya marehemu mpenzi wake walipoulizwa wanasemaje kuhusu hiyo hukumu walijibu kwamba wameridhika walau Oscar akae lupango. Inasemekana Oscar anaweza kukaa jela miezi 10 kumi na baadaye kuachiwa kwa kifungu cha nje. Wengi walitaka Oscar walau angehukumiwa miaka 10 jela. Wengi hawajaridhika na hukumu hiyo na hasa weusi. Wengi walitegemea Jaji Judge Thokozile Masipa, ambaye amewahi kuamua kesi kadhaa hapo nyuma na kutoa hukumu kali, angeweza kumudhibu Pistorius vikali. Lakini wengine wanamtetea Jaji Masipa kwamba yeye kama Jaji asingeweza kutoa hukumu kutokana na maoni ya jamii na msukumo wa wadau mbalimbali katika kesi hii bali kwa kufuata misingi ya sheria na jinsi waendesha mashitaka walivyowakilisha hii kesi mbele ya mahakama.

Cha msingi hapa ni kwamba waendesha mashitaka wa Serikali ya Afrika Kusini walishindwa kudhihiri kupita mashaka yoyote kwamba Pistorius alimuua mpenzi wake Reeva kwa makusudi yaani kwa kudhamiria. Kwa kawaida makosa ya jinai mtu hushitakiwa na jamuhuri yaani raia wote wa nchi husika. Ili kuondoa shaka ya kumwonea mtu mmoja basi ni sharti nyinyi mlio wengi mdhihirishe pasi kuwa na mashaka yoyote kwamba ni kweli huyu mtu alitenda kosa. Na katika makosa ya jinai kudhibitisha dhamira ya kosa ni jambo la msingi kabisa. Mimi najitenga kumlaumu Jaji Masipa kwamba amekuwa na upendelevu, la hasha. Nawarudishia mzigo waendesha mashitaka kwamba walishindwa kujenga msingi wa kesi ya Pistorius vizuri na hasa walipoona mwelekea wa utetezi ni kutia matundu ili kuonyesha Pistorius hakuwa na dhamira ya kumuua mpenzi wake na badala yake alimuua kwa bahati mbaya akidhani anaua mvamizi (intruder). Kinyume chake nawapongeza Wanasheria watetezi wa Pistorius kwa umahiri wao.

Kidogo hii inafanana na kesi ya mcheza mpira maarufu bwana O.J. Simpson miaka nikiwa mwanafunzi Chuo kikuu. Ilikuwa kesi kama novo vile. Simpson ni kweli kimazingira alimuua mkewe, lakini watetezi wake walijaribu kutia mashimo kwenye ushahidi hata ule wa DNA hadi OJ akashinda ile kesi. Inauma haki inapopitia mtihani kama huu. Mtu kauawa lakini mwisho wa siku hakuna anayewajibishwa kulingana na uzito wa kosa. Inasemekana mtu wa kwanza kuua ni jamaa mmoja alkiwa akiitwa Kaini. Huyu jamaa aliua mdogo wake tena kwa wivu tu. Kesi yake ilivyoenda katika msahafu alipewa adhabu na Mungu japo siyo ya kunyongwa. Lakini adhabu hiyo iliambatana na ulinzi pia ili wengine wasije wakajichukulia sheria mkononi kama inavyotokezea nyakati zetu hizi.

Hiki ndicho kitu huwa kinanitatiza katika tasnia ya sheria. Nilipenda sana niwe mwanasheria wakati fulani lakini nikawa napata shida kumtetea mtu ambaye kuna wakati nitakuwa nina uhakika kwamba ni mkosaji.

Labada inafanana na tunavyojifunza katika msahafu wa Biblia kwamba Yesu Kristo anasimama badala yetu akitutetea kwa Mungu. Akisema damu yake alimwaga pale msalabani Golgota kwa ajili yetu, tumekiri na kutubu hivyo Mungu atusamehe tu. Niwatie moyo wanasheria waendelee na kazi hii nzuri ya kuwatia adabu wavunja sheria lakini pia kuwatetea hao hao wakosaji ama wakionyesha hawana makosa, au kama wamekosa wasamehewe au wapewe adhabu wanayoweza kustahimili.

Hayo ndiyo maoni yangu kwa kesi ya Oscar Leonard Carl Pistorius, kijana mashuri japo kaonyesha kuwa mtata sana.

Ibara alizozikataa Mwanasheria mkuu wa Zanzibar – zisome kwa makini

October 1, 2014 § Leave a comment

Eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

2.-(1) Eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni:

(a) eneo lote la Tanzania Bara, ikiwa ni pamoja na eneo lake la bahari

ambalo kabla ya Muungano lilikuwa likiitwa Jamhuri ya Tanganyika

pamoja na maeneo mengine yatakayoongezeka; na

(b) eneo lote la Zanzibar, ikiwa ni pamoja na eneo lake la bahari ambalo

kabla ya Muungano lilikuwa likiitwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar

pamoja na maeneo mengine yatakayoongezeka.

(2) Rais wa Jamhuri ya Muungano atakuwa na mamlaka ya kuigawa

Jamhuri ya Muungano katika mikoa, wilaya na maeneo mengine na kwa upande

wa Zanzibar, Rais anaweza kukasimu mamlaka hayo kwa Rais wa Zanzibar.

(3) Kwa madhumuni ya ibara ndogo ya (1), Bunge litatunga sheria

itakayoainisha na kufafanua mipaka ya eneo la Jamhuri ya Muungano.

 

9.-(1) Katiba hii ni sheria kuu katika Jamhuri ya Muungano kwa mujibu

wa masharti yaliyowekwa na Katiba hii.

(2) Kwa madhumuni ya ibara ndogo ya (1), endapo masharti ya sheria

yoyote itakayotungwa na vyombo vyenye mamlaka ya kutunga sharia yatatofautiana na masharti ya Katiba hii, masharti ya sheria hiyo yatakuwa batili

na yatatenguka kwa kiwango kile kinachotofautiana na masharti ya Katiba hii.

(3) Mtu yeyote, chombo au taasisi ya Serikali, jumuiya, wakala yeyote

na mamlaka binafsi zitakuwa na wajibu wa kuzingatia na kutii masharti ya

Katiba hii na sheria za nchi.

(4) Sheria yoyote, mila, desturi au uamuzi wowote wa chombo cha dola

au ofisa wa Serikali ni sharti ufuate na kuzingatia masharti yaliyomo kwenye

Katiba hii na kwamba sheria, mila, desturi au uamuzi wowote ambao

hautawiana au kwenda sambamba na masharti ya Katiba hii utakuwa batili.

(5) Serikali itaweka utaratibu wa kuwawezesha wananchi kuifahamu, kuilinda na kuitii Katiba hii.

86.-(1) Katika uchaguzi wa Rais kila chama cha siasa

kitakachotaka kushiriki katika uchaguzi wa Rais, kitawasilisha kwa Tume

Huru ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Muungano, kwa mujibu wa sheria, jina la

mwanachama mmoja anayependekezwa kwa nafasi ya madaraka ya Rais.

(2) Endapo ni mgombea huru, kwa kuzingatia sifa zitakazoainishwa

katika sheria itakayotungwa na Bunge atawasilisha jina lake kwenye Tume Huru

ya Uchaguzi.

(3) Mapendekezo ya majina ya wagombea katika uchaguzi wa Rais

yatawasilishwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi katika siku na kwa utaratibu

utakaoainishwa katika sheria.

(4) Endapo itafika siku na saa iliyotajwa kwa ajili ya

kuwasilisha mapendekezo ya majina ya wagombea, ni mgombea mmoja tu

ambaye anapendekezwa kuwa halali, Tume Huru ya Uchaguzi itawasilisha jina

lake kwa wananchi, nao watapiga kura ya kumkubali au kumkataa

kwa mujibu wa masharti yaliyoainishwa katika Katiba hii na sheria.

(5) Uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano utafanyika siku

itakayoteuliwa na Tume Huru ya Uchaguzi kwa mujibu wa sheria.

(6) Mgombea wa nafasi ya madaraka ya Rais atatangazwa kuwa

amechaguliwa kuwa Rais iwapo atapata kura zaidi ya asilimia hamsini ya

kura zote halali zilizopigwa kwa nafasi ya madaraka ya Rais.

(7) Endapo katika uchaguzi wa Rais hakuna mgombea

aliyekidhi masharti ya ibara ndogo ya (6), basi uchaguzi utarudiwa ndani

ya siku sitini kwa wagombea walioshika nafasi ya kwanza na ya pili na

mgombea atakayepata kura zaidi ya asilimia hamsini atatangazwa kuwa

mshindi wa nafasi ya urais.

(8) Mambo mengine yote yahusuyo utaratibu wa uchaguzi wa Rais

yatakuwa kama itakavyofafanuliwa katika sheria itakayotungwa na Bunge kwa

ajili hiyo.

  1. Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itakuwa na muundo wa Serikali

mbili ambazo ni:

(a) Serikali ya Jamhuri ya Muungano; na

(b) Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Utekelezaji wa shughuli za Mamlaka ya Nchi

71.-(1) Shughuli zote za Mamlaka ya Nchi katika Jamhuri ya Muungano

zitatekelezwa na kudhibitiwa na vyombo viwili vyenye mamlaka ya utendaji,

vyombo viwili vyenye mamlaka ya utoaji haki, na pia vyombo viwili vyenye

mamlaka ya kutunga sheria na kusimamia utekelezaji wa shughuli za umma.

(2) Vyombo vyenye mamlaka ya utendaji vitakuwa ni Serikali ya

Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar; vyombo vyenye

mamlaka ya utoaji haki vitakuwa ni Mahakama ya Jamhuri ya Muungano na

Mahakama Kuu ya Zanzibar, na vyombo vyenye mamlaka ya kutunga sheria na

kusimamia utekelezaji wa shughuli za umma vitakuwa ni Bunge na Baraza la

Wawakilishi.

(3) Kwa ajili ya utekelezaji bora wa shughuli za umma katika Jamhuri

ya Muungano, na kwa ajili ya mgawanyo wa madaraka juu ya shughuli hizo

baina ya vyombo vilivyotajwa katika Ibara hii, kutakuwa na Mambo ya

Muungano kama yalivyoorodheshwa katika Nyongeza ya Kwanza ya Katiba hii

na pia kutakuwa na mambo yasiyo ya Muungano, ambayo ni mambo mengine

yote yasiyo ya Muungano.

(4) Kila chombo kilichotajwa katika Ibara hii kitaundwa na kutekeleza

majukumu yake kwa kufuata masharti mengine yaliyomo katika Katiba hii.

Mamlaka ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano

  1. Serikali ya Jamhuri ya Muungano itakuwa na mamlaka ya utekelezaji

katika Jamhuri ya Muungano kwa Mambo ya Muungano na kwa mambo yote

yasiyo ya Muungano yanayohusu Tanzania Bara.

Mamlaka ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mambo yasiyo ya Muungano

73.-(1) Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itakuwa na mamlaka na haki

juu ya mambo yasiyo ya Muungano yanayohusu Zanzibar.

(2) Bila kuathiri mipaka iliyowekwa na Katiba hii, katika kutekeleza

mamlaka yake chini ya ibara ndogo ya (1), Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar

itakuwa na uwezo na uhuru wa kuanzisha uhusiano au ushirikiano na jumuiya au

taasisi yoyote ya kikanda au kimataifa.

(3) Endapo, katika kutekeleza mamlaka na majukumu yake kwa mujibu

wa Ibara hii, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itahitaji kupata ushirikiano

kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa ajili ya kufanikisha uhusiano au

ushirikiano na jumuiya au taasisi ya kikanda au kimataifa, Serikali ya Jamhuri

ya Muungano yaweza kufanikisha uhusiano au ushirikiano huo kwa kuzingatia

masharti ya Katiba hii na sheria itakayotungwa na Bunge.

(4) Kwa madhumuni ya Ibara hii, Bunge litatunga sheria itakayoainisha

na kufafanua:

(a) majukumu na mipaka ya utekelezaji wa mamlaka ya Serikali ya

Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhusu

uhusiano au ushirikiano wa kikanda au kimataifa;

(b) utaratibu wa kushughulikia athari zinazotokana na uhusiano au ushirikiano wa kikanda au kimataifa;

(c) utaratibu wa utafutaji na upatikanaji wa mikopo na misaada

kutokana na uhusiano au ushirikano huo;

(d) utaratibu au masharti ya kuvunja au kuimarisha uhusiano au

ushirikiano huo;

(e) utaratibu wa mawasiliano na mashauriano kati ya Serikali ya

Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhusu

uhusiano au ushirikiano wa kikanda au kimataifa;

(f) utaratibu wa utekelezaji wa masharti ya Ibara hii; na

(g) mambo mengine yatakayohusu uhusiano au ushirikiano wa kikanda

au kimataifa chini ya Ibara hii.

Mahusiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar

74.-(1) Katika kutekeleza majukumu yake katika maeneo mbalimbali,

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itazingatia misingi ya

kushirikiana na kushauriana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa lengo la

kukuza na kulinda maslahi ya Taifa na maendeleo ya wananchi.

(2) Kwa madhumuni ya kukuza umoja na uhusiano, Serikali ya

Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano, zinaweza

kushauriana na kushirikiana katika mambo yanayohusu uongozi, utawala,

vyombo vya uwakilishi na mahakama.

(3) Utendaji wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Serikali ya

Mapinduzi ya Zanzibar au chombo chochote cha Serikali hizo utatekelezwa kwa

kuzingatia umoja wa Jamhuri ya Muungano na wajibu wa kukuza utaifa.

(4) Bila kuathiri masharti ya Ibara hii, Serikali ya Jamhuri ya Muungano,

kwa makubaliano maalum baina yake na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,

inaweza kutekeleza jambo lolote lililo chini ya mamlaka ya Serikali ya

Mapinduzi ya Zanzibar kwa mujibu wa makubaliano hayo.

Wajibu wa viongozi wakuu kulinda Muungano

75.-(1) Bila kuathiri wajibu wa kila raia uliotajwa katika Katiba hii, kila

kiongozi mkuu mwenye mamlaka ya utendaji katika Jamhuri ya Muungano

aliyetajwa katika ibara ndogo ya (3) atakuwa na wajibu, katika kutekeleza

madaraka aliyopewa kwa mujibu wa Katiba hii, kuhakikisha kuwa anatetea,

analinda, anaimarisha na kudumisha umoja wa Jamhuri ya Muungano wa

Tanzania.

(2) Kwa madhumuni ya masharti ya ibara ndogo ya (1) kila kiongozi

mkuu aliyetajwa katika ibara ndogo ya (3), kabla ya kushika madaraka yake,

ataapa kuutetea, kuulinda na kuudumisha Muungano kwa mujibu wa Katiba hii.

(3) Viongozi wakuu wanaohusika na masharti ya Ibara hii ni:

(a) Rais wa Jamhuri ya Muungano;

(b) Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano;

(c) Rais wa Zanzibar;

(d) Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano; na

(e) Makamu wa Rais wa Zanzibar.

Madaraka ya kutunga Sheria

128.-(1) Mamlaka yote ya kutunga sheria juu ya mambo mengine yote

yahusuyo Tanzania Bara, yatakuwa mikononi mwa Bunge.

(2) Mamlaka yoyote ya kutunga sheria katika Zanzibar juu ya mambo

yote yasiyo ya Muungano yatakuwa mikononi mwa Baraza la Wawakilishi.

(3) Endapo sheria yoyote iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi inahusu

jambo lolote katika Zanzibar ambalo liko chini ya mamlaka ya Bunge, sheria hiyo

itakuwa batili na itatanguka na pia endapo sheria yoyote iliyotungwa na Bunge

inahusu jambo lolote ambalo liko chini ya mamlaka ya Baraza la Wawakilishi,

sheria hiyo itakuwa batili na itatanguka.

(4) Sheria yoyote iliyotungwa na Bunge kuhusu jambo lolote haitatumika

Zanzibar isipokuwa kwa mujibu wa masharti yafuatayo:

(a) Sheria hiyo iwe imetamka wazi kwamba itatumika Tanzania Bara na

vilevile Zanzibar au iwe inabadilisha, kurekebisha au kufuta sheria

inayotumika Zanzibar;

(b) Sheria hiyo iwe inabadilisha au kurekebisha au kufuta sheria

iliyokuwa inatumika tangu zamani Tanzania Bara ambayo ilikuwa

inatumika pia Zanzibar kwa mujibu wa Mapatano ya Muungano wa

Tanganyika na Zanzibar, ya mwaka 1964, au kwa mujibu wa sheria

yoyote ambayo ilitamka wazi kwamba itatumika Tanzania Bara na

vilevile Zanzibar; au

(c) Sheria hiyo iwe inahusu Mambo ya Muungano, na kila inapotajwa

Tanzania katika Sheria yoyote ifahamike kuwa sheria hiyo itatumika

katika Jamhuri ya Muungano kwa mujibu wa ufafanuzi uliotolewa na

masharti ya Ibara hii.

5) Bila kuathiri kutumika kwa Katiba ya Zanzibar kwa mujibu wa Katiba

hii kuhusu mambo yote ya Zanzibar yasiyo Mambo ya Muungano, Katiba hii

itakuwa na nguvu ya sheria katika Jamhuri nzima ya Muungano na endapo sheria

nyingine yoyote itakiuka masharti yaliyomo katika Katiba hii, Katiba ndiyo

itakuwa na nguvu, na sheria hiyo nyingine, kwa kiasi inachokiuka Katiba,

itakuwa batili.

Utaratibu wa

kubadilisha Katiba

129.-(1) Bunge linaweza kutunga sheria kwa ajili ya kubadilisha masharti

yoyote ya Katiba hii kwa kufuata kanuni zifuatazo:

(a) Muswada wa sheria kwa ajili ya kubadilisha masharti ya Katiba hii au

masharti yoyote ya sheria yanayohusu jambo lolote isipokuwa mambo

yanayohusu aya ya (b) au (c), utapitishwa kwa kuungwa mkono kwa

wingi wa kura za Wabunge wote;

(b) Muswada wa sheria kwa ajili ya kubadilisha masharti yoyote ya

Katiba hii au masharti yoyote ya sheria yoyote yanayohusika na jambo

lolote kati ya mambo yaliyotajwa katika Nyongeza ya Pili, utapitishwa

tu iwapo utaungwa mkono kwa kura za wabunge ambao idadi yao

haipungui theluthi mbili ya Wabunge wote wa Tanzania Bara na

theluthi mbili ya Wabunge wote wa Zanzibar;

(c) Muswada wa sheria kwa ajili ya kubadilisha masharti yoyote

yanayohusika na jambo lolote kati ya mambo yaliyotajwa katika

Nyongeza ya Tatu iliyoko mwishoni mwa Katiba hii, utapitishwa tu

iwapo utaungwa mkono kwa zaidi ya nusu ya kura halali zilizopigwa

na wananchi wa Tanzania Bara, na zaidi ya nusu ya kura halali

zilizopigwa na wananchi wa Tanzania Zanzibar katika kura ya maoni

itakayoendeshwa na kusimamiwa na Tume Huru ya Uchaguzi kwa mujibu wa sheria.

(2) Kwa madhumuni ya ufafanuzi wa masharti ya ibara ndogo ya (1)

kubadilisha masharti ya Katiba hii maana yake ni pamoja na kurekebisha au

kusahihisha masharti haya au kufuta na kuweka masharti mengine badala yake au

kusisitiza au kubadilisha matumizi ya masharti hayo.

Where Am I?

You are currently viewing the archives for October, 2014 at kadulyu.