Matamko ya viongozi wa dini na hatima ya katiba tunayoitaka Tanzania

August 1, 2014 § Leave a comment

Nilikuwa nasita sana kusema juu kinachoendelea sasa kuhusiana na katiba. Kuna hisia naanza kuzipata kuhusu matamshi ya viongozi wa dini kuhusu kuonekana mkwamo wa mchakato wa katiba.

Imekuwa sasa ni kawaida kwa viongozi wa dini kutoa matamko yenye mwelekeo fulani hasa katika mambo ya kisiasa. Matamko mengi tuliyosikia yamekuwa yakitolewa wakati wa uchaguzi au kwenye matukio ya uvunjifu wa amani au vurugu za kisiasa na hasa zihusuzo harakati ya vyama vya upinzani upande mmoja na serikali/CCM upande mwingine. Sina haja ya kupitia hayo matamko maana sote huwa twayasikia.

Ukifuatilia mwanzoni mwa mchakato wa katiba taasisi za kidini za kikristo na kiislam zilitoa matamko ya kuasa Rasimu ya katiba yaTume – almaarufu Tume ya Warioba ndiyo ijadiliwe na bunge la katiba. Hii ni mara tu baada ya hotuba ya Rais kuleta mtafaruku pale bungeni na kuonyesha kwamba chama tawala walikuwa na mapendekezo mbadala ambayo waliyaingiza kwa kisingizio kwamba Bunge la Katiba lina mamlaka (mandate) ya kubadili au kuingiza mambo mapya katika katiba pendekezwa.

Matamko haya ya mwanzo yalitia moyo watanzania kwamba viongozi wa dini wako na jamii na wako tayari kusimamia maslahi mapana ya nchi.

Sote twajua kilichotokea pale bungeni baada ya wabunge wa chama tawala kuwa na msimamo wa pamoja kukataa baadhi mapendekezo ya tume ya katiba. Upinzani nao wakaungana kuunda UKAWA (Umoja wa (kutetea) Katiba ya Wananchi). Hatimaye wakatoka bungeni kwa kuona kwamba huenda wakatumika kama muhuri wa kuhalalisha katiba ambayo itakuwa kinyume na matakwa ya wananchi.

Baada ya mapumziko ya bunge la katiba kupisha bunge la bajeti, tumeshuhudia msimamo wa UKAWA kutokurudi bungeni. Baadaye ndiyo tukaanza kusikia tena matamshi ya viongozi wetu wa dini. Yamegawanyika katka makundi kadhaa: wengine wakimlaumu Rais, wengine wakitaka maridhiano ya pande mbili wengine wakiwasihi UKAWA wabadili msimamo wao.

Wakati wa sikukuu ya Eid tumesikia viongozi wakiwataka UKAWA warudi bungeni. Kinachonishangaza viongozi wetu hawashauri kwa uwazi yakinifu kitu chochote kuhusu yale mambo yaliyowafanya UKAWA wakatoka nje na kususia bunge. Baadhi ya ninayokumbuka ni:
1.Bunge kujadili serikali mbili wakati zilizopendezwa na tume ni tatu.
2. Matumizi ya ubabe na lugha za kutukanana
3. Ubaguzi wa rangi kwa baadhi ya wabunge
4. Mkakati wa wabunge wa chama tawala kukataa mapendekezo ya msingi ya rasimu ambayo yana lengo la kubadili mfumo wa utawala na uwajibikaji nchini.

Hili la nne kwa upana linachukua pia la kwanza.

Ni vizuri kwa viongozi kusaidia kuielekeza jamii pale wanapoona kuna tatizo na hasa lenye uwezo wa kuathiri jamii nzima. Lakini ni muhimu sana kwa viongozi wa dini kuepa siasa za vyama na kusimamia haki tu.

Tatizo lililopo sasa hivi ni ushawishi unaofanywa na wanasiasa kuvuta hisia za mirengo ya kidini kwenye katiba. Hili linafanywa makusudi. Nitaeleza kwa nini.

Msimamo wa chama tawala ni kwamba sheria ya mabadiliko ya katiba inatoa nafasi ya bunge la katiba kubadilisha au hata kuingiza mambo mapya kabisa katika rasimu. Wanafanya hivyo ili kupata mwanya wa kubadili mambo ya msingi yaliyopendekezwa likiwamo hili la serikali tatu. Kwa muda mrefu sasa tumekuwa na mjadala wa kuwa na mahakama ya kadhi ndani ya mfumo wa utoaji haki. Kimekuwa kilio cha muda sasa. Na kuna wakati chama tawala kiliahidi kwenye ilani yake ya uchaguzi kwamba kitalifanyia kazi lakini kwa sababu ya ama shinikizo kutoka kwa baadhi ya viongozi wa dini zingine au kwa sababu inazozijua yenyewe haijaweza kulitekeleza hilo.

Tume ya katiba pia haikuweka hilo ndani ya katiba imetoa sababu za kutokufanya hivyo tunaweza tukakubali au kutokubali hizo sababu na mapendekezo yake. Bila shaka kwa msimamo wa wabunge wa chama tawala tayari inatumika kama njia ya kushawishi umma kwamba kwa msimamo huo mambo mapya likiwemo na la mahakama ya kadhi vinaweza kuingizwa. Na hivyo kuanza kuonyesha kuwa wale wanaosimamia kujadili rasimu ya tume ni kama wanafanya nafasi ya kuingiza mambo haya mapya iwe finyu au isiwepo kabisa. Na hii inaweza kuelezea sura ya mwelekeo wa maoni ya viongozi wa dini kwa sasa.

Ni kwa mara nyingine tena tunataka kushuhudia wananchi tugawanywa kwa misingi ya dini zetu kwa jambo hili nyeti la katiba. Ni propaganda mbaya sana kwa taifa letu. Swala la mahakama ya kadhi linajadilika vizuri bila kuathiri misingi ya katiba iliyopendekezwa. Ni maoni yangu yangu kwamba viongozi wetu wa dini wasimamie haki ili rasimu iliyotokana na maoni yaliyokusanywa kutoka kwetu ndiyo ijadiliwe. Kama wabunge wameshindwa kufikia mwafaka kuhusu muundo wa muungano waje watuulize wananchi tutawaambia muundo tunaoutaka siyo siri, tunajua tunachokitaka labda tu kama wanakiogopa.

Katika kiwango cha raia sie wa Bara na visiwani ni marafiki na mara nyingi huwa tunajadili mfumo tunaoutaka ili kurahisisha maisha na mwingiliano wetu kibiashara na kijamii. Wanasiasa wana mambo yao huenda yanaweza kuwa mbali na tunachotaka. Napenda kumnukuu mzee Warioba anaposema, walipowaona viongozi wa siasa kupata maoni yao walijikita zaidi kwenye power yaani madaraka na si masilahi mapana yetu wananchi. Tukitaka mambo ya manufaa kwetu wanaona yanahatarisha maslahi yao. Na hilo ndilo linalosababisha mgogoro huu tulio nao. Viongozi wa dini ndio wako karibu na sisi wanajua shida zetu na haja zetu maana wanaziombea kila siku. Hizo ndizo ningeomba wazisimamie.

Advertisements

Tagged:

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

What’s this?

You are currently reading Matamko ya viongozi wa dini na hatima ya katiba tunayoitaka Tanzania at kadulyu.

meta

%d bloggers like this: