Uoga aliousema Nyerere ukihusianisha na utungaji wa katiba mpya
February 24, 2014 § 1 Comment
Dada https://www.facebook.com/MariaSarungi ametoa leo nukuu kutoka nukuu ya Mwl JK Nyerere, ‘Uongozi wetu na Hatma ya Tanzania’. Ikisema hivi “Hatuwezi kuachia utamaduni wa woga ukawa ni mbinu au sifa mpya ya uongozi. Na sasa lazima tukiri kwamba utamaduni huu wa woga unaanza kuwa sehemu ya tatizo letu la kitaifa… Viongozi wetu hivi sasa wanaogopa kutumia nguvu za hoja ili kufikia maamuzi muhimu. Kwa sasa wanatumia hila zaidi kuliko hoja; vitishio kwao ni mbinu rahisi zaidi kuliko adha ya kutumia akili na kupata hoja safi ya kumjibu mpinzani katika mjadala… Na kama tukiacha utamaduni wa woga ukazagaa tutakuwa tunakaribisha udikteta. Uhuru hauji wala haudumishwi bila kuwa tayari kulipa gharama zake; na vitu vyote vyenye thamani kubwa gharama yake ni kubwa”
Marafiki kadhaa wametoa maoni yao lakini baadaya kuyasoma nika na maoini yafuatayo: tafadhali fuatana nami.
https://www.facebook.com/joseph.ngwegwe Nildhani nukuu aliyoitoa https://www.facebook.com/MariaSarungi imetoa ujumbe wazi kabisa kwa muktadha wa wakati tulio nao na changamoto zinazotukabili. Uoga unaozungumziwa si wa kufanya fujo. Kiuhalisia nukuu inapinga fujo na mbinu za kuzima hoja pinzani bali kujenga hoja juu ya hoja.
Ngoja nitoe mfano: juzi Waziri Mkuu alinukuliwa na vyombo vya habari akisema yeye na chama chake ukiwaamsha usiku kutoka kwenye usingizi mzito, hata ukiwakurupusha wataamka na kusema muundo wa dhati wanaoutaka ni wa serikali mbili. Tungetegemea kwa uelewa wake na nafasi yake katika jamii kwanza angetambua jambo hili kuwa ni nyeti kwa maana kwamba tume imekusanya maoni kutoka kwetu na wengi tuliotoa maoni tulitaka serikali tatu – kupindua ukweli huu kwa kutumia mgongo wa chama ni kitu Nyeti (sensitive) sana.
Pili angejenga hoja ya kisayansi kwa nini yeye binafsi anaona mfumo wa serikali mbili ndio utajenga muungano zaidi. Akizingatia uzoefu wake na hasa pale aliposema bungeni kuwa Zanzibar si nchi nini kilichomtokea.
Tatu aeleze kwa nafasi yake na uzoefu wake katika ngazi ya juu ya uongozi wa nchi hii ni kitu gani ambacho atakifanya tofauti na zamani ili muungano wa serikali mbili uwe bora kuliko sasa na kuliko wa hata wa serikali tatu hata moja.
Nne yeye kwa nafasi yake anamshaurije Rais kuhusu madhara ya kupinga msingi wa katiba mpya. Akijua kabisa kwamba kuondoa serikali tatu kunaweza kusababisha rasimu ya sasa kufutika na kuhitaji kuandika rasimu isyozingatia matakwa ya watu? Kama kuna hoja kwamba tume ilituchakachulia maoni isemwe wazi kuonyesha kinyume na matokeo waliyoyatangaza. Yaani kwamba waliotaka serikali mbili ni wengi kuliko waliotaka serikali tatu au moja. Hatuna haja ya kujadili Rasimu iliyochakachuliwa. Na kama haikuchakachuliwa basi iachwe ipimwe kwenye kura ya maoni. Chama tawala kina serikali na mvuto wa kutosha tu waitishe bunge libadili sheria ya kutunga katiba mpya iruhusu kampeni wakati kura ya maoni watushawishi wananchi tubadili maamuzi yetu.
Tano anatabirije matukio yatakayotokea ikiwa wananchi tutaikataa katiba iliyowekewa mambo ambayo hatukuyataka?
Rais amesikika akisema tusipokubaliana, katiba ya zamani itaendelea na tusijidanganye kwamba kutakuwa na serikali ya mpito akiongeza kuwa yeye atakuwa Msogaaaa! Akipumzika. Waziri Mkuu anatumiaje nafasi yake kumshauri Rais kwamba kama wananchi wakikataa katiba yenye mapendekezo yaliyolazimishwa na chama tawala kiuhalisia wamekikataa chama tawala na kuendelea kutawala ni kufanya hivyo kinyume na taratibu za demokrasia? Ametumiaje muda wake na nafasi yake kumshauri kuwa zoezi hili la kutunga katiba ukishalipeleka kwa wananchi ni irreversible yaani huwezi kurudi nyuma labda tu kwa kutumia mabavu hadi pale katiba wanayoitaka wengi itakapopatikana?
Ili tufanikiwe kupata katiba mpyaTujenge hoja kwa hoja badala ya kuogopa na kukwepa mawazo mbadala na matokeo yake unaanza kuwatisha watu kwa kuwa wewe una nguvu.