Je, Chama halali cha siasa au cha kiraia kina haki ya kuhoji/kupinga mchakato wa katiba?

May 6, 2013 § Leave a comment

Haya ni mawazo yangu kutokana na hoja ya Mwanakijiji aliyoweka kwenye facebook http://www.facebook.com/mwanakijiji/posts/10151507173841156?comment_id=25255265&offset=0&total_comments=101 akizungumzia mchakato wa katiba na tishio la Chadema kujitoa kwenye mchakato huo kama mambo fulani fulani wanayoyaona yana kasoro hayatafanyiwa kazi. Nimesoma maoni ya watu wengi nikasukumwa kuandika maoni haya:

Ndugu yangu Mimi Mwanakijiji hali ya kukubali kusikiliza hoja za vyama vya upinzani kwa mtizamo chanya bado. Ukiangalia mawazo ya kila mtu unaona jinsi ambavyo mfumo wa chama kimoja umetuathiri namna tutazamavyo vyama vingine. Wengi huenda hawajui kwamba vyama vyote vya siasa vina haki sawa tofauti tu kimoja kinaongoza serikali. Ni utaratibu wetu kisiasa kwamba demokrasia ya wengi ndiyo sauti inayotawala. Mfumo ambao ni mzuri tu na unasaidia kuondoa migogoro ya kisiasa.

Bado wengi hata ndani ya chama tawala wanaona vyama vingine ni viovu na vinataka kuwatendea waTanzania mambo yasiyofaa na hivyo siasa za kupakana matope na hata kutaka kuangamizani zimeanza kujitokeza. Huenda ni kwa sababu elimu ya uraia ni ndogo watu wengi tumeleweshwa na mvinyo wa ukiritimba wa mfumo wa chama kimoja. Inatufanya tuone chama chenye sauti mbadala ni adui anayetakiwa kuondolewa. Hii ni sumu mbaya kwa watanzania tusipoiondoa itatuletea shida huko mbele ya safari.

Tungeelewa uhalali wa mfumo wa vyama vingi tusingeshangaa Chadema kuuona kasoro mchakato wa katiba. Ukweli tu wa kawaida ni kwamba Chama tawala kina maslahi ya moja kwa moja katika mchakato huu wa kuleta katiba mpya na itashangaza sana kama kitaacha kuthibiti utaratibu ili katiba ijayo kwa namna fulani au namna ya moja kwa moja isaidie Chama tawala kuendelea kuwa madarakani kwa miaka mingine 50.Vyama vingi viliruhusiwa nchini kwa utaratibu huu huu, kwamba tukiacha vije kwa nguvu ya mabadiliko yaliyokuwa yanaukumba ulimwengu (hasa ule wa kijamaa) Chama tawala kingekosa uthibiti na huenda ingekuwa ndo njia ya kuondoka madarakani. Kwa hiyo ni busara ya kawaida kwa status quo yoyote duniani. It is good to stage-manage the change rather than being overwhelmed by it.

Watanzania wengi hatuko kwenye vyama hivi vya siasa lakini tunavisikiliza hoja zake kwa makini. Chama tawala kinaweza ku-stage-manage lakini hatupendi kipitilize, nani atatuambia kinapitiliza? Bila shaka ni vyama vya upinzani au haya mashirika ya kiraia. Hatuwezi kufanya kazi hii mmoja mmoja, itafanyika ndani ya mfumo huu wa kisiasa tulio nao.

Ili kuleta katiba itayoleta ulinganifu ni muhimu basi kuyasikiliza makundi mengine yanayotambulika kisheria. Na popote pale duniani mfumo mzuri wa mabadiliko ya kisiasa haukuletwa na status quo bali vyama vya kisiasa pinzani na vyama na mashirika ya kiraia wakiweka agenda zao mbele ya raia na kuungwa mkono. Wale wanaopinga utaratibu wapewe nafasi Watanzania wawasikie na hasa vyama vya siasa na mashirika ya kiraia. Wananchi hatuwezi mmoja mmoja kutengeneza agenda, tunaweza kupitia taasisi au zaidi sana kupiga kura. Chama tawala wasiwe na wasiwasi waache Chadema na wengine waseme kile wanachokiona kina kasoro. Watanzania tutaelewa.

Mwisho hii kusema jambo hili si la kisiasa si sahihi, katiba ni jambo la kisiasa. Siasa ni mfumo wa nchi na raia wake namna ambavyo wanajiendesha. Siasa ni pana sana. Tusidhani kuwa siasa ni pale tu mtu anapoita watu Jangwani (sasa hivi sijui itakuwa wapi) na kusema jambo. Ni mfumo wa jinsi watu wanavyoishi na nchi inavyojiendesha. Tulipata uhuru kwa njia za kisiasa si kwa mtutu wa bunduki. Tunataka katiba mpya tuipate kwa njia za kisiasa pia si kwa njia ya bunduki. Hivyo mtu kuibuka na kusema hili si jambo la kisiasa ni kusema kitu ambacho hakina mantiki. Kama CCM wanadhani mchakato wa katiba ni sahihi na rasimu iliyoko mezani ni nzuri watumie njia za kisiasa kufanya hivyo kuwashawishi watanzania. Kama Chadema au chama kingine wanaona kuna tatizo nao wako huru kutumia njia za kisiasa kufanya hivyo. KATIBA NI JAMBO LA KISIASA na mfumo wa kuitunga upya na hata kuipigia kura ni siasa ‘pure’. Na siasa ni nzuri siyo kitu kibaya. Kuifanya nchi yetu ibadilike kila mtu sasa hivi anatakiwa awe mwana siasa. Tumefanya dhambi kuiacha siasa kwa watu wachache na kuwaita eti wao ndio wanasiasa. Halafu mambo yakienda mrama tunawalaumu, tunawaonea, tuliwaweka wenyewe. Siasa ni jukumu la kila mtanzania tusiwaachie kakundi ka watu. Tuwasikilize kama hoja zao zinakidhi mahitaji na maslahi yetu tuwaunge mkono kama la tukatae. Wepewe nafasi badala ya kuwashetanisha kabla hawajatoa hoja zao. Kumbuka ninyi nyote (CCM, CHADEMA, CUF, NCCR, UDP, TLP, n.k) ni vyama vyetu sisi Watanzania, mmoja wenu tulimpa madaraka hadi 2015 tu!

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

What’s this?

You are currently reading Je, Chama halali cha siasa au cha kiraia kina haki ya kuhoji/kupinga mchakato wa katiba? at kadulyu.

meta

%d bloggers like this: