Mkurugenzi wa National Housing Corporation afanye nini?
March 1, 2013 § Leave a comment
Mkurugenzi Mkuu/Mtendaji wa NHC siyo IHC ni mtu namheshimu sana kwa elimu yake, ueledi na hekima ya uongozi aliyojaliwa na Mwenyezi Mungu. Si Mtu wa kukurupuka hata kidogo. Wengi wetu ni kijana mwenzetu pia. Na tumekuwa tukijivunia kwamba vijana wanaweza, tuwape tu nafasi na kuacha kutangaza matangazo ya kazi kwamba eti uzoefu miaka 15!
Ninaamini atajirudi na kuheshimu maoni ya walio wengi maana sauti ya wengi ni sauti ya Mungu. Ni kweli NHC hawatutendei haki wananchi wa Tanzania. Kuna miradi mingine ya NHC inasukumwa na matakwa ya kisiasa zaidi kuliko hali halisi. Na hii ndiyo inayoangusha mashirika yetu ya umma. Tulitiwa matumaini na ujio wa Kijana mwenzetu pale NHC lakini pia wengine tulipatwa na wasiwasi kama kweli angeendelea na kutunza ueledi na umakini wa utendaji wake ndani ya bahari ya mivutano ya kimaslahi ya baadhi wanasiasa.
Mivuto ya kisiasa na kusikiliza wakubwa itakuwa ngumu kwake kupingana nayo. Lakini bado kuna nafasi ya kusimama walau kutimiza makusudi ya mwanzo ya NHC. Tulikuwa na makazi hapo Magomeni, Ilala, n.k ya watu wa kipato cha chini. Magomeni wamevunja tayari, mpango nini hasa? wanajenga sijui nini pale? Mimi sielewi! Hivi viongozi wetu wanadhani mtu wa kipato cha chini anaweza kununua nyumba ya shs millioni 40? Ukikopa kwa miaka 15 utajalipa shs ngapi mwisho wa mkopo? Kuna riba hapo, watu hawaambiwi kinaga ubaga. Benki gani itakopesha bila uhakika wa mambo haya mawili: kwanza dhamana pili uwezo wa kulipa sehemu ya deni na riba yake kila mwezi.
Benki ziko kufanya biashara ati. Labda siyo Benki! Ningeshauri kwanza tukubaliane na hii misamiati, maana yake nini: Mtu wa kipato cha chini, mtu wa kipato cha juu, tajiri na siku hizi kuna fisadi. Fisadi nadhani ni mtu mwenye mali nyingi lakini ukifuatilia hujui kazipata wapi, zingine anaweka nje ya nchi pia. Fisadi nadhani tunamfahamu. Lakini tafsiri ya hao wengine kila mmoja ana maana tofauti. Baada ya kujua maana ya hayo maneno tufanye utafiti kuwa na hakika kweli tuna hawa watu. Kwa mfano nina mashaka sana kama tuna watu hawa wanaoitwa ‘middle class”. Watanzania wengi hata wenye kazi za ajira hawana kipato endelevu. Kwa mfano ni watanzania wangapi wanaoweza kukaa nyumbani kwa miezi mitatu mfululizo nyumbani kutokana labda na tatizo fulani na familia ikandelea kuishi maisha ya kiwango kilekile. Wengi wetu tunaitumikia fedha hatujafikia kiwango cha pesa kututumikia sisi. Tunaona kila siku dhamana walizoweka watu zinapigwa minada, familia zinafukuzwa na kuachwa ukiwa. Benki hazina huruma hata kidogo. Tusiwatie watanzania matumaini hewa kwa sarakasi ya kwenye vyombo vya habari, tuwaambie ukweli.
Mwisho namuomba Mkurugenzi wa NHC aache hasira atulie na kutambua uhuru wa wananchi kutoa maoni yao halafu aje na nguvu ya hoja tujadiliane. Hii nadhani ni nafasi adhimu ameipata kusikiliza upande wa pili wanasemaje. Na akivuka hapa tutakuwa na NHC ambayo ni rational inayoendeshwa kwa kukidhi hali halisi na mahitaji ya watu ambayo kwayo ilianzishwa.
Kama kiongozi anayeheshimika aweke mfano mzuri wa kusikiliza hata maoni pingamizi. Akiwa aggressive kupambana na kuzima mawazo mbadala haitoi nyota njema kwake. Kwa sababu katika ukinzani wa mawazo ndio tunaweza kupata kitu bora. Waziri wa ardhi alipokuwa UN alikuwa akitoa mawazo mazuri sana, amerudi nyumbani sasa, tumaini letu ataweka hayo mawazo katika vitendo halisi.